Wakati  mume wa mwimba Injili Bongo,  Flora Mbasha, Emmanuel Mbasha 
akiachiwa huru kwa dhamana kufuatia kesi ya kudaiwa kumbaka shemejiye, 
Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima la jijini Dar es Salaam, Josephat
 Gwajima ameibuka na kunena mazito kuhusiana na sakata hilo.
Mbasha aliachiwa kwa dhamana juzi akitokea Gereza la Keko, Dar baada ya 
kupandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza katika Mahakama ya Wilaya ya 
Ilala, Juni 17, mwaka huu na kusomewa mashitaka mawili ya ubakaji ambayo
 hata hivyo, aliyakana.
ILIVYOKUWA KORTINI
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, mheshimiwa Wilbeforce Luago
 siku hiyo ya Juni 17, alitoa hoja kwamba upande wa jamhuri hauna 
pingamizi hivyo dhamana ipo wazi.
Alisema mshitakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili, mfanyakazi wa 
serikali na wa kutoka katika taasisi inayotambulika sanjari na shilingi 
milioni 5 kila mmoja. Mshitakiwa alishindwa kutimiza masharti hayo siku 
hiyo hadi hadi juzi alipotimiza, akaachiwa.
Mwendesha mashitaka wa mahakama hiyo ambaye ni wakili wa serikali, 
Nassoro Katuga bila kuchelewa aliitaja kesi hiyo yenye namba CC/186/2004
 ambapo rafiki wa Mbasha aliyejitambulisha kwa jina la George Mushi na 
baba wa mtuhumiwa aitwaye Mwahimu Juma ndiyo waliofanikisha dhamana 
hiyo. Kesi yake itatajwa tena Julai 17, 2014.
GWAJIMA SASA
Akizungumza na mwanahabari wetu juzi wakati Mbasha akiwa nje kwa 
dhamana, Mchungaji Gwajima alieleza namna ambavyo sakata hilo 
limeitikisa Injili nchini Tanzania kutokana na kuibuka kwa madai mengi 
likiwemo suala la Flora kusemekana amehamia nyumbani kwake kitu ambacho 
alikipinga.
Gwajima alisema anasikitika sana kuona ndoa ya Flora na Emmanuel Mbasha 
inatikisika akizingatia Flora ni muumini wake hivyo moja kwa moja ugomvi
 wao unaonekana kutia dosari mwenendo mzima wa uinjilishaji katika 
jamii.
“Naumizwa sana na sakata hili lakini hivi karibuni niliamua kuwaita 
ndugu wa pande zote mbili (Flora na Mbasha) nikazungumza nao kwa kirefu 
na tukamaliza tofauti zote lakini tatizo likabaki lile la kisheria zaidi
 (mashitaka ya ubakaji kwa Emmanuel),” alisema Gwajima ambaye makao 
makuu ya kanisa lake yapo Kawe jijini Dar.
AANDAA TAMKO ZITO
Mchungaji Gwajima alisema kutokana na sakata hilo kugusa Injili, 
ameandaa tamko zito ambalo atalitoa rasmi atakaporudi safari yake ambayo
 hakueleza anakokwenda.
“Hatuwezi kukaa kimya juu ya hili, nasafiri lakini nikirudi tu nitatoa tamko rasmi kwa kuwaalika waandishi wa habari,” alisema.
IBADANI JUMAPILI
Katika hatua nyingine, ndani ya ibada ya kanisa hilo iliyofanyika 
Jumapili iliyopita, Mchungaji Gwajima alitumia dakika kama 15 katika 
mahubiri yake kutupa kile kilichodaiwa kuwa ni jiwe gizani ambapo wengi 
waliamini ni kuhusiana na sakata hilo.
“Mimi siyo kama wale, sijibu hoja kama zile, mfano ukiwa unaoga halafu 
chizi akachukua nguo zako na ukamkimbiza nani ataonekana chizi? Tatizo 
la Watanzania ni kuwa wakisikia kitu kipya kinaanza kwao badala ya 
kukithamini wanakididimiza ili kisiendelee, lakini mimi siyo kama wao,” 
alisema.
Aliongeza: “Mimi kila mwaka naenda Japan na ninawa-lecture Wajapani 
ambao pia huja hapa kanisani zaidi ya 40 kila mwaka na mwaka huu 
watakuja Septemba, lakini Watanzania hawashtuki na kuja kujifunza juu ya
 ufufuo wa wafu wengi wao wanakalia kuandika stori kwenye magazeti 
lakini mimi siyo kama wale.”
AMEFUNGUKIA SAKATA LA MBASHA?
Ingawa Mchungaji Gwajima hakueleza moja kwa moja kuhusu tukio la Mbasha 
lakini maneno hayo yalitafsiriwa kwamba ni ya kujibu hoja zinazomhusisha
 yeye na tukio hilo.
Anaendelea:”Mimi nimehubiri nchi zaidi ya 53 duniani na nyingi za Ulaya 
na Marekani halafu mtu amekaa Magomeni miaka yote anatengeneza stori ya 
gazeti, unatarajia niijibu, mimi siyo kama wale nimetumwa na nina kazi 
natakiwa kuifanya duniani na siwezi kufa mpaka niimalize.”
“Inawezekana mlishawaangamiza wengi kabla ya mimi, kwa kuwatungia stori 
hizo za uongo lakini mimi siyo kama wale na mwezi huu wa nane 
ninaendelea na mkutano Iringa, waache waandike lakini mimi ni chombo 
kingine na siyo kama wale.”
DONGO GIZANI?
Baadhi ya waumini waliokuwa katika ibada hiyo, walibaki njia panda na 
katika giza nene ingawa wengi waliamini alitupa vijembe katika sakata la
 Mbasha haswa alipokuwa akisema, ‘mimi siyo kama wale’.