Lowassa Atangaza ‘Uamuzi Mgumu’
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Lomooti, Kata ya Lolkisale wilayani humo alipokwenda kutembelea boma la kisasa la mfugaji Isaya Lembekure, Lowassa alisema haiwezekani wananchi wa Monduli kukosa ardhi wakati, kuna ardhi yao iliyohodhiwa na wachache bila kuendelezwa.
“Monduli tumechoka na uuzwaji wa ardhi. Kila mahali ni matatizo ya uuzwaji wa ardhi. Sasa tunatangaza kuanza mchakato wa kuyarejesha mashamba yote ya wawekezaji ambayo hayajaendelezwa. Tayari hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa ili kuyarejesha,” alisema Lowassa.
Tamko hilo la Lowassa, lilipokewa kwa shangwe na wananchi wa Wilaya ya Monduli na limekuja wakati migogoro ya ardhi baina ya wawekezaji na wananchi na wakulima na wafugaji imeshamiri nchini.
Licha ya kutoa agizo hilo, Lowassa ameendelea kukemea uuzajiwa wa ardhi wilayani humo, unaofanywa kinyume cha taratibu na Serikali.
“Kuanzia sasa kiongozi wa kijiji atakayebainika kuhusika kuuza ardhi kinyemela, ang’olewe kupitia mikutano ya vijiji,” alisema Lowassa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Monduli, Twalib Mbasha alisema tayari halmashauri hiyo imeanza maandalizi ya kuyarejesha mashamba hayo kwa kuwataka wahusika wa mashamba hayo kujieleza kwa nini hawajayaendeleza hadi leo.
“Halmashauri inakusudia kuyafuta mashamba yote yasiyoendelezwa na yaliyotelekezwa, hii ni kutokana na kushindwa kufuata masharti ya ardhi kama ilivyoanishwa na sheria ya Ardhi namba 4,999 fungu la 44 na fungu la 48. Nimetoa siku 90 watu hawa wajieleze,” alisema Mbasha.
Aliyataja mashamba yanayotarajiwa kurejeshwa kwenye mamlaka za Serikali za Vijiji kuwa ni Meru Enterprises namba 10, ACU LTD namba 2390, TANFORM LTD 47, TANFORM 44 na Melembuki Kitesho Mollel namba 974 katika Kijiji cha Lolkisale.
Mashamba mengine ni The Monduli Parents Sec School, Musa Mamuya namba 2278 lipo Makuyuni, David Pello 2275, Hillary Gadi namba 2474, Khalifan Said Masoud 2276, Masoud Said Masoud 2277 yapo Kijiji cha Mswakini Juu.
Alitaja pia yaliyopo katika kijiji hicho ni ya Lucas Petro Kambei namba 2597 na Rungwa game Safari Ltd namba 2765.
Alisema mashamba mengine ni Omary Daudi Mshana 1571, Saidi Rashid Lena namba 2549 yaliyopo Kijiji cha Naitolia, wakati mashamba mengine ni ya T.R Msuya namba 3, Esimingori Estate Ranch namba 7/2, Saburi Estate Ltd namba 7, Musa Y. Mamuya yaliyopo Makuyuni
0 maoni:
Chapisha Maoni