BAADHI ya Watanzania wanaoishi Ulaya na Marekani wamesema Tanzania
inakosa mapato mengi kutokana na gharama za kupiga simu nchini kuwa
ghali karibu mara tatu ya viwango vya nchi zote za Afrika Mashariki.
Wamesema kuwa inawabidi kutumia ujanja wa kupiga simu nchini kupitia
nchi jirani kama vile Kenya na Uganda ili kukwepa mzigo wa gharama za
kuunganishwa ili kuwasiliana moja kwa moja na ndugu zao nchini.
“Sisi kama Watanzania tunaopenda kuisaidia ndugu na nchi yetu kwa
ujumla kwa sasa tunaona kero kupiga simu za moja kwa moja kwa sababu
gharaa za uunganishaji simu zinazoingia Tanzania moja kwa moja kutoka
hapa (Ulaya) ni ghali sana,” alisema mmoja wa watanzania anayeishi
nchini Marekani.
Alielezea mtindo wa Watanzania wengi wanaoishi ugaibuni kuona njia
rahisi ni kuunganishwa simu kwa kupitia kampuni za simu za Kenya au
Uganda zinaipunguzia mapato Tanzania na kunufaisha nchi jirani.
“Katika hili nani anapoteza?” Alihoji Mtanzania huyo na kujibu:
“Tanzania kama nchi ndiyo inayoathirika kwa sababu tu ya gharama kubwa
za uunganishaji simu za ughaibuni. Kwa sasa simu zinazopigwa kuja huko
Tanzania zinapitishiwa Kenya na Uganda, hivyo mapato yanaenda kwa nchi
hizo.”
Alifafanua kuwa nchi hizo jirani zinafaidika mara mbili, kwanza kwa
kuunganisha simu kuingia nchini kwao na pili kuzielekeza tena kwenda
Tanzania.
Pamoja na mzunguko huo, Watanzania hao wanadai ni njia yenye gharama nafuu zaidi kuliko kupiga simu za moja kwa moja nchini.
Akizungumza kwa kuwawakilisha Watanzania wenzake wa huko Ughaibuni
ambao wamekuwa wakisononeshwa na jambo hilo, waliitaka Mamlaka ya
Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuingilia kati suala hilo ili uchumi wa nchi
usiendelee kuhujumiwa.
Alisema mara kadhaa wamewasiliana na TCRA bila mafanikio na uchunguzi
wao wa awali ulibaini kuwa kampuni za simu nchini zinapewa uhuru wa
kujipangia viwango vya gharama za kuunganisha simu zinazoingia nchini.
Gharama za simu
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kupitia kampuni za simu nchini
Marekani za Rebtel, Wisecalling na VIP, umedhihirisha wazi kuwa
malalamiko ya Watanzania hao yana hoja ambayo serikali kupitia TCRA
inapaswa kuingilia kati.
Kwenye mtandao wa kompyuta wa kampuni hizo ulionyesha wazi viwango
vya gharama za kuunganisha simu Tanzania ni aghali kuliko nchi nyingine
za Afrika Mashariki.
Gharama hizo ambazo zimo kwa kiwango cha senti za dola za Marekani
kwa kila sekunde ambayo muongeaji anatumia wakati anaunganishwa na simu
kwa ukanda wa Afrika Mashariki ziliainishwa kama ifuatavyo.
Kampuni ya Rebtel kupiga simu Tanzania kupitia simu za mezani na
mkononi ni 25, Kenya 8 kwa simu za mezani na 10 kwa simu za mkononi,
Uganda 12 simu za mezani na 13 za mkononi, Rwanda 15 mezani na mkononi
wakati Burundi mezani na mkononi ni 14.
Kampuni ya VIP kwa Tanzania simu za mezani 24 na mkononi 25 wakati
Kenya ni 9 kwa mezani na mkononi ni 12, Uganda ni 13 kwa mezani na
mkononi, Rwanda 16 mezani na 18 mkononi wakati Burundi 12 mezani na 18
mkononi.
Kampuni ya Wisecalling kwa Tanzania ni 14 mezani na 24 mkononi wakati
Kenya ni 6 mezani na 10 mkononi, Uganda 6 mezani na 17 mkononi, Rwanda
16 mezani na 13 mkononi na Burundi 7 mezani na 13 mkononi.
Meneja Uhusiano wa TCRA, Innocent Mungy alipoulizwa kuhusu suala hilo
alisema mamlaka hiyo haina uwezo wa kudhibiti gharama zinazotozwa kwa
simu zinazoingia kwenye mitandao ya hapa nchini.
“Sisi (TCRA) tuulizeni gharama za viwango vya kupiga simu kwa kampuni
zetu za ndani, maana kisheria ndiko mamlaka yaetu yanakoishia, lakini
kuhusu simu zinazoingia kutoka nje sisi hatuna mamlaka ya
kuziingilia,”alisema Mungy na kuongeza:
“Kuna kampuni kubwa tano zilizopewa leseni gateway (kupokea simu za
kimataifa) na kuziingiza kwenye mtandao wa hapa nchini, sasa TCRA
haiwezi kufahamu ni kiwango gani zinachotozwa kampuni za simu za ndani
katika kupata huduma hiyo, na wao wanawatoza vipi wateja wa huko”.
Maelezo hayo ya Mungy yanamaanisha kwamba TCRA wana uwezo wa kisheria
wa kudhibiti viwango vinavyotozwa kwa simu zinazopigwa kutoka nchini
pekee, lakini gharama ya simu zinazoingia kutoka nje ya nchi zimeachwa
mikononi mwa kampuni za simu husika.
Alhamisi, 19 Juni 2014
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
0 maoni:
Chapisha Maoni